Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Watumishi
wa Umma mkoani Iringa wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa
wanapowahudumia wananchi ili wananchi wanufaike na huduma wanazopatiwa.
Rai
hiyo ilitolewa na Afisa Uchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa, Evarist Shija alipowasilsiha mada juu ya
mapambano dhidi ya rushwa mahala pa kazi kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa hivi karibuni.
Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa akifuatilia mada ya Evarist Shija kutoka Takukuru Iringa |
Shija
alisema kuwa rushwa ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma, mali ya umma na
dhamana aliyonayo mtu kwa niaba ya umma na akaamua kuitumia kwa manufaa yake
binafsi. Alisema kuwa tendo la rushwa hutokea pale mtumishi anapoamua
kupindisha sheria na taratibu za nchi kwa nia ya kujipatia fedha au kitu
chochote chenye thamani hata kama kitu hicho kina thamani ndogo. Alisema kuwa
kutokana na hali hiyo, watumishi wa umma wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya
rushwa na viashiria vyovyote vya vitendo hivyo katika utumishi wao. “Mpokea rushwa huwa katika nafasi yenye
mamlaka au nafasi ya kutoa maamuzi yatakayo muathiri anayetoa rushwa. Rushwa
hutokea katika utumishi wa umma na hata katika sekta binafsi” alisisitiza
Shija.
Shija
alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya
mwaka 2007, imeharamisha vitendo vya rushwa kuwa jinai na inayataja makosa ya
rushwa bayana.
Akiongelea
kanuzi za maadili, Afisa uchunguzi huyo aliyataja maadili kuwa ni sheria,
taratibu na kanuni zilizokubalika katika jamii au kundi kama muongozo wa
mahusiano kati yao na namna wanavyoendesha maisha yao. “Kanuni hizi zinatambulisha mambo mazuri ya kufanya dhidi ya yale mabaya
yasiyostahili kufanywa na kwa kila unalotenda kuna tuzo au adhabu yake. Hivyo,
kila mtumishi wa umma ana wajibu wa kufuata kanuni za maadili katika utendaji
wake wa kazi” alisisitiza Shija.
Shija
aliyataja maadili hayo kuwa ni uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria
na matumizi sahihi ya taarifa. Aidha, alizitaja kanuni za maadili ya viongozi
na watumishi wa umma kuwa ni kutoa huduma bora kwa wananchi, utii kwa serikali
na wananchi wake, kuwa na bidii ya kazi na kutoa huduma bila upendeleo. Kanuni
nyingine ni kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria na
matumizi sahihi ya taarifa.
Akiongelea
umuhimu wa kuzingatia maadili na kuepuka vitendo vya rushwa kwa watumishi wa
umma, Shija alisema kuwa ni kuendelea kujenga imani ya wananchi juu ya uadilifu
wa serikali yao na kuondoa migongano ya kimahusiano kazini. Kuhakikisha
yanakuwepo matumizi mazuri ya fedha na rasilimali nyingine na kuleta tija kwa
kuongeza thamani ya fedha katika miradi na huduma zinazotolewa. Vilevile,
kufuata maadili ni muhimu katika kudhibiti mianya ya rushwa na ukiukwaji wa
maadili, kuleta tija mahali pa kazi na kudhibiti matumizi ya madaraka
waliyonayo viongozi na watumishi.
Maadhimisho
ya wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2017 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo
‘kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika utoaji huduma: vijana washirikishwe
kuleta mabadiliko barani afrika’. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa inaadhimisha
wiki ya Utumishi wa Umma tarehe 16-23/6/2017 kwa kutembelea watumishi wa makao
makuu ya mkoa, Ofisi za Wakuu wa Wilaya na hospitali ya rufaa ya Mkoa na kutoa
mada mbalimbali zinazohusu haki na wajibu wa mtumishi wa umma, mapambano dhidi
ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, mapambano dhidi ya rushwa na kusikiliza na
kutatua kero za watumishi.
=30
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni