Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Halmashauri ya wilaya ya Mufindi
yapongezwa kwa kupata hati safi ya ukaguzi kwa hesabu za serikali zilizoishia Juni,
2016 na kutakiwa kudumisha ushirikiano ili rasilimali za Halmashauri ziendelee
kutumika kwa manufaa ya wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa na mkuu wa mkoa
wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake aliyoitoa katika kikao cha baraza
la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kujadili taarifa ya mdhibiti na
mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2016
wilayani Mufindi.
Masenza
alisema “mheshimiwa mwenyekiti, nichukue fursa hii kwa namna
ya pekee kabisa kuipongeza Halmashauri ya wilaya ya Mufindi kwa kupata hati
safi ya ukaguzi kwa hesabu za serikali zilizoishia tarehe 30 Juni, 2016.
Hongereni sana”.
Aliitaka Halmashauri
hiyo kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya madiwani na watendaji wa
Halmashauri ili rasilimali za Halmashauri ziwanufaishe wananchi. Aidha,
aliitaka Halmashauri hiyo kuendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya udhibiti
wa ndani ili iweze kupata hati safi kila mwaka.
Mkuu wa mkoa wa Iringa aliitaka Halmashauri
hiyo kuhakikisha hoja zote za miaka ya nyuma zinafanyiwa kazi na kuhakikiwa na
na kufungwa na mkaguzi wa hesabu za Serikali. “Kwa mujibu wa taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu
wa hesabu za Serikali Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ina hoja 27 za miaka ya
nyuma ambazo hazijafungwa na hoja 11 ambazo zimejirudia mwaka 2015/2016” alisema Masenza.
Mkuu wa mkoa aliitaka Halmashauri kuweka utaratibu
wa kulipa madeni yanayofikia shilingi 1,269,395,971 yaliyotokana na madai ya wakandarasi,
watoa huduma na watumishi kama ilivyobainishwa kwenye taarifa ya mdhibiti na mkaguzi
wa hesabu za Serikali. Alishauri mawasiliano yafanyike na Serikali kuu kuona
uwezekano wa kulipa sehemu ya deni hilo. Vilevile, aliitaka Halmashauri hiyo
kulipa deni la shilingi 193,711,438.40 ambalo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani
kwenda mfuko wa wanawake na vijana kiasi ambacho hakikupelekwa mwaka 2015/2016.
“Madeni yote ya miaka ya nyuma ya mifuko
hii yalipwe ipasavyo kwa kuzingatia agizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)” alisisitiza Masenza.
Kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri
ya wilaya ya Mufindi kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali
kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2016 wilayani Mufindi ni utekelezaji wa
agizo la waziri mkuu alilolitoa tarehe 22/4/2017 katika kikao kazi cha baraza
la mawaziri cha kujadili taarifa ya ukaguzi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa
hesabu za Serikali ya mwaka 2015/2016.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni