Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Halmashauri ya
wilaya ya Iringa imetakiwa kujikita katika kuwasilisha usahihi wa mapato zaidi
ya shilingi 400,000,000 yatokanayo na vyanzo vyake jambo lililoisababishia
kupata hati isiyoridhisha.
Agizo hilo
lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake kwenye
kikao cha baraza la madiwani la Halmshauri ya wilaya ya Iringa kujadili taarifa
ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa hesabu zilizoishia tarehe
30 Juni, 2016 kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Masenza alisema
“tofauti na hesabu za mwaka 2014/2015,
ambapo Halmashauri yenu ilipata hati safi, katika hesabu za 2015/2016
Halmashauri yenu imepata hati isiyoridhisha. Hii ni changamoto
kwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Aidha, eneo ambalo lilisababisha msifanye
vizuri ni; mkaguzi kushindwa kuthibitisha usahihi wa mapato ya kiasi
shilingi 401,554,383 yaliyotokana na vyanzo mbalimbali vya Halmashauri kutokana
na kukosekana kwa risiti 38 katika mfumo wa kitabu cha ukusanyaji mapato ya fedha
taslimu (MRECOM). Ni imani yangu kuwa, eneo hilo litafanyiwa kazi ipasavyo ili
kutoruhusu hali hiyo kujitokeza katika kaguzi zijazo”.
Mkuu wa mkoa wa
Iringa aliitaka Halmashauri ya wilaya ya Iringa kufanyia kazi hoja zote za
miaka ya nyuma na kufungwa na mkaguzi wa hesabu za serikali wa mkoa. “Kwa mujibu wa
taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa ina hoja 39 za miaka ya nyuma ambazo hazijafungwa na hoja 7
ambazo zimejirudia 2015/2016. Hii ni idadi kubwa ya hoja inayohitaji kuweka
mpango kazi wa kuzishughulikia na kuhakikisha hoja zote zinafungwa” alisema Masenza.
Aidha, aliitaka Halmashauri ya wilaya ya Iringa
kuweka utaratibu wa kulipa madeni yanayofikia kiasi cha shilingi 1,900,180,524 yaliyotokana
na madai ya wakandarasi, watoa huduma na watumishi kama yalivyobainishwa na
mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali. Aidha, aliitaka Halmashauri hiyo
kulipa deni la kiasi cha shilingi 78,647,303 ambazo ni asilimia 10 ya mapato ya
ndani kwenda mfuko wa wanawake na vijana kiasi ambacho hakikupelekwa kwenye
mifuko husika kwa mwaka 2015/2016.
Aliagiza madeni yote ya miaka ya nyuma ya
mifuko hii yalipwe kwa kuandaa mpango kazi wa ulipaji wa madeni hayo kama
inavyosisitizwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC).
Akiongelea udhibiti wa mifumo ya ndani, mkuu wa
mkoa aliitaka Halmashauri kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani ili watumishi
wasiostahili kulipwa mishahara na malipo mengine hawalipwi.
“Taarifa ya mdhibiti
na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali imeonesha kuwa kiasi cha shilingi
2,070,000 kimelipwa kwa watumishi wasiostahili kwa kuwa walikuwa tayari
wamestaafu kwa mujibu wa sheria. Aidha, jukumu la Halmashauri katika hili ni
kuhakikisha kuwa, wote waliolipwa kimakosa wanarejesha kiasi hicho kilicholipwa
kimakosa” aliagiza Masenza.
Vilevile, aliitaka Halmashauri kupata uthibitisho
kutoka Hazina wa kurejeshwa kwa kiasi cha shilingi 16,471,109 ambacho
hakikulipwa kwa watumishi kutokana na sababu mbalimbali za kiutumishi.
Kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri
ya wilaya ya Iringa kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali
kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2016 wilayani Iringa ni muitikio wa
agizo la waziri mkuu alilolitoa tarehe 22/4/2017 katika kikao kazi cha baraza
la mawaziri cha kujadili taarifa ya ukaguzi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa
hesabu za Serikali ya mwaka 2015/2016.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni