Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Serikali
imejipanga kukabiliana na changamoto za elimu maalum kwa shule za msingi na
sekondari mkoani Iringa kwa kuanza imepeleka shilingi milioni 300 ili
kuwawezesha watoto kusoma katika mazingira mazuri na rafiki.
Kauli hiyo
ilitolewa na waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
alipotembelea shule ya msingi Mtwivila iliyopo katika Manispaa ya Iringa juzi.
Prof. Ndalichako
alisema kuwa elimu maalumu nchini inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo
wizara yake haiwezi kuzimaliza kwa siku moja. Alisema kuwa katika kukabiliana
na changamoto hizo, wizara yake ilipeleka mkoani Iringa shilingi milioni 300 kwa
ajili ya shule za msingi na sekondari zenye mahitaji maalumu.
Akiongelea
changamoto ya fedha za nauli kwa watoto wa shule ya msingi Mtwivila yenye
watoto wenye mahitaji maalum pindi shule inapofungwa, Prof. Ndalichako
aliwataka wazazi kuwapa kipaombele watoto hao kwa kuwapatia nauli ili waweze
kurudi nyumbani shule zinapofungwa.
Aidha, alitatoa wito kwa jamii kununua
bidhaa zinazotengenezwa na watoto wanaosoma elimu maalumu kama njia ya kuunga
mkono juhudi zao.
Akishukuru kwa
ziara ya waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina
Masenza alisema kuwa ziara hiyo imewajengea uwezo watoto wenye mahitaji maalumu
na kujiamini zaidi katika masomo yao.
Aidha, alimtaka Katibu Tawala mkoa wa Iringa
kusimamia vifaa vyote vilivyotolewa na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili viweze kuwanufaisha watoto
wote mkoani Iringa.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni