Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Serikali
imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa mitambo, magari na
madawa ya kuzimia moto ili kukabiliana na uhaba wa vifaa kwa Jeshi la Zimamoto
na uokoaji nchini.
Kauli
hiyo ilitolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji nchini, Thobias
Andengenye alipokuwa akikabidhiwa funguo za gari la Zimamoto na mkuu wa mkoa wa
Iringa lililotolewa na Zacharia HansPope katika kituo cha Zimamoto katika
Manispaa ya Iringa jana.
Kamishna
Andengenye alisema “kwa mwaka wa fedha
2016/2017 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ununuzi
wa magari mawili ya kuzimia moto na kwa mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi
bilioni tatu zimetengwa kwa ajili hiyo. Hii ni dalili njema sana na inaonesha
jinsi Serikali ilivyo na nia ya dhati ya kuondoa kabisa kama siyo kupunguza kwa
kiasi kikubwa upungufu wa vitendea kazi katika Jeshi la Zimamoto na uokoaji”.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Austria na
Ubeligiji ambazo zimeonesha nia ya kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za
kimarekani 5,000,000 19,000,000 mtawalia kwa ajili ya mitambo na vifaa vya kuzimia
moto.
“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa ndugu
Zacharia HansPope, kwa kutoa msaada wa gari aina ya Mercedes Benz lenye ujazo
wa lita 5,000 za maji. Huu ni msaada mkubwa sana kwa Jeshi la Zimamoto na
uokoaji na mkoa wa Iringa” alisema Kamishna Andengenye. Aliongeza kuwa gari
lililokuwa linahudumia katika mkoa wa Iringa lilipata ajali gharama ya
matengenezo ni kubwa sana. Aidha, alitoa rai kwa wakazi na wafanyabiashara
katika mkoa wa Iringa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na uokoaji hasa
wanapoweza kusaidia vifaa ili kuboresha huduma za Zimamoto na uokoaji za kuokoa
maisha na mali za wananchi.
Akiogelea
matukio ya moto na maokozi, Kamanda wa Zimamoto mkoa wa Iringa, Mrakibu Kennedy
Komba alisema kuwa mwaka 2015/2016 matukio ya moto na maokozi yalikuwa 110
ambapo matukio ya moto yalikuwa 90 na matukio ya maokozi ni 20 sawa na 1.1%.
Mwaka 2016/2017 matukio ya moto na maokozi yalikuwa 97, ambapo matukio ya moto
yalikuwa 83 na matukio ya maokozi yalikuwa 14 sawa na 0.97%. “Kwa ukumla mwaka 2015/2016 na mwaka
2016/2017 kuna upungufu wa matukio kwa 0.13%” alisema Mrakibu Komba.
Mrakibu
Komba alisema kuwa upungufu wa matukio ya moto na maokozi unatokana na juhudi
za maofisa na askari kufanya ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto kwa njia
mbalimbali. Alizitaja njia hizo kuwa ni elimu kwa umma kwa njia ya vyombo vya
habari.
Aliongeza kuwa ofisi yake imeanzisha programu kabambe ya kupitia shule
zote za msingi na sekondari katika Manispaa ya Iringa kutoa elimu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni