Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Waziri
wa maliasili na utalii amevunja bodi ya jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori
Pawaga na Idodi (Mbomipa)
na
kuelekeza katiba ipitiwe upya na kufanyiwa marekebisho yatakayoinufaisha
jumuiya hiyo na wananchi kwa ujumla.
Waziri
wa maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe alitoa kauli hiyo jana katika
kijiji cha Tungamalenga alipofanya ziara ya kikazi katika wilaya ya Iringa.
Prof.
Maghembe alisema “hakuna bodi ya Mbomipa,
kuanzia leo naivunja rasmi bodi ya Mbomipa. Lazima tujipange kujenga bodi mpya
ya Mbomipa. Tutengeneze katiba mpya ya Mbomipa ili iendane na sheria ya
wanyamapori na kanuni za wanyamapori. Aliongeza kuwa mkinzano wa katiba ya Mbomipa
na sheria ya wanyamapori imetoa mwanya kwa bodi kushindwa kutekeleza majukumu
yake kikamilifu.
Waziri
huyo alitoa siku 20 kwa wataalam wakiongozwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya
wilaya ya Iringa kupitia upya katiba hiyo na kuiboresha ili iendane na matakwa
ya sheria na kanuni za wanyamapori nchini. Alielekeza kuwa baada ya rasimu hiyo
kukamilika baraza la ushauri la wilaya, jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori
Pawaga na Idodi, mkurugenzi wa wanyamapori, mhifadhi mkuu wa Tanapa na afisa
wanyamapori wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa wakutane na kuipitia rasimu hiyo
ya katiba ili ipitishwe.
Prof.
Maghembe alisema kuwa baada ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, mikataba yote iliyokuwa
imeingiwa na bodi iliyopita imevunjwa rasmi. Aidha, aliagiza wawekezaji wote
wenye nia ya kuwekeza katika eneo hilo wafuate utaratibu unaokubalika kisheria.
Alishauri kuwa bodi inapopitisha mikataba ishauriwe na wanasheria wa mkoa.
Nae
mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliwataka watakaogombea nafasi katika Mbomipa
kujipima kwanza uadilifu wao kabla ya kuamua kugombea. Alisema kuwa tatizo
kubwa katika Mbomipa ni udanganyifu.
“Hakuna
hata kijiji kimoja kati ya vijiji 21 vinavyounda jumuiya ya hifadhi ya
wanyamapori Pawaga na Idodi kilichonufaika na uwepo wa jumuiya hii. Wawekezaji wengi
walioingia mikataba na Mbomipa wamekuwa matapeli” alisema Masenza.
Aliongeza kuwa serikali imeendelea kuhakikisha mbomipa inakuwepo ili kusaidia
kudhibiti ujangili katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha na maeneo yanayozunguka
hifadhi hiyo.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni