Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Jamii
imetakiwa kujivunia nchi na rasilimali zilizopo pamoja na vivutio vya utalii na
kuvilinda ili viwe endelevu.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa wilaya ya Mufindi, Jamhuri William aliyemuwakilisha
mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika usiku wa Utalii Karibu Kusini uliofanyika
katika chuo cha ualimu Kreluu mjini Iringa jana.
William
alisema kuwa jamii ya mikoa ya nyanda za juu kusini inatakiwa kujivunia nchi
yao na rasilimali zilizopo hasa utunzaji na uhifadhi wa vivutio vya utalii.
“Utalii ni uzalendo, lazima tujivunie nchi
yetu na rasilimali tulizonazo. Vivutio vya utalii vyote tunavyoviona na
kuvisikia ni sehemu ya rasilimali muhimu za nchi ambazo lazima tuzitunze ili
nazo zituletee uchumi” alisema William.
Mkuu
wa wilaya ya Mufindi alishauri rasilimali vivutio vya utalii kuhifadhiwa na
kutunzwa ili visiharibiwe na kutoweka. “Katika
utunzaji wa vivutio vya kitalii, ndiyo vitatuletea fedha nyingi na hatimae
kukuza uchumi wa nchi yetu” alisema William.
Alisema
kuwa serikali imeamua kuutangaza utalii kisayansi ili ulete matokeo kwa
wananchi. Aliwaomba wananchi kuwa sehemu ya kutangaza utalii ili kuleta
mafanikio makubwa zaidi.
Akitoa
maoni yake, mwanafunzi wa chuo cha ualimu Kreluu, Yuster Tweve alisema kuwa
usiku wa Utalii Karibu Kusini ni fursa nzuri ya kuwakutanisha wadau mbalimbali
pamoja na kujadili fursa zilizopo katika sekta ya utalii. Alishauri kuwa usiku
wa utalii uwe unafanyika siku zote za maonesho ya Utalii Karibu Kusini ili
wadau mbalimbali wapate nafasi ya kukaa na kubadilishana mawazo yatakayochangia
katika kukuza utalii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni