Jumapili, 1 Oktoba 2017

SEKTA YA UTALII YAENDELEA KUKUA KILA MWAKA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Sekta ya utalii imekuwa ikikuwa na kuchangia katika mapato ya Taifa zaidi ya dola za kimarekani milioni 2,000 mwaka 2016.

Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa kufungua maadhimisho ya siku ya utalii Duniani, maonesho ya Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) mjini Iringa jana.
 
Prof. Jumanne Maghembe (Mb)
Prof. Maghembe alisema kuwa mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola za marekani milioni 1,353.29 mwaka 2011 hadi kufikia dola za marekani 2,131.57 mwaka 2016. 

Mapato haya yamechangiwa na watalii wa kimataifa waliotembelea nchini ambao waliongezeka kutoka watalii 867,994 mwaka 2011 hadi kufikia watalii 1,284,279 kwa kipindi hicho. Takwimu zinaonesha kuwa sekta hii inachangia zaidi ya 11% ya ajira zote hapa nchini” alisema Prof. Maghembe.

Akiongelea mchango wa utalii katika ukuaji wa uchumi, waziri huyo alisema kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazochangia sana ukuaji wa uchumi nchini. 

“Nyote mtakubaliana na mimi kwamba, utalii ni moja kati ya sekta inayochangia ukuaji wa uchumi nchini kutokana na kuwa chanzo cha kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Utalii huongeza ajira na kipato kwa jamii, pia ni chachu kwa ukuaji wa sekta zingine. Sekta hii huchangia 25% ya mauzo nchi za nje.

Prof. Maghembe alisema kuwa ukuaji wa sekta ya utalii nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za serikali katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali, utangazaji, mazingira bora ya uwekezaji pamoja na ushirikiano madhubuti baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Nae mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake daima utakuwa mstari wa mbele kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ya mfano na kukua kwa kasi.

=30= 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...