Na Mwandishi Maalum Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Mkoa wa Iringa umejizatiti
kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu ili waanze matibabu mapema na kuzuia ugonjwa
huo kuambukiza wengine.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu
wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akizindua kampeni tambuzi
za kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza katika uwanja wa kumbukumbu ya Samora
mjini Iringa jana.
Mheshimiwa Masenza alisema “njia kuu ya kuzuia kuenea kwa kifua kikuu ni
mgonjwa kugunduliwa mapema pale anapoanza kuonyesha dalili za awali na kuwekwa
katika matibabu bila kuchelewa. Mgonjwa mmoja anaweza kuwaambukiza watu
wasiopungua 20 kwa mwaka. Bila ya kuweka juhudi za kuwapata wagonjwa mapema na
kuwatibu, kifua kikuu kitaendelea kuenea na kuwamaliza watu wengi nchini”.
Alisema kuwa kwa kipindi cha Januari 2016-Juni 2017, mkoa wa Iringa umeweza
kugundua wagonjwa wapatao 455. Alisema kuwa kwa lengo la Manispaa ya Iringa ni
kupima na kugundua watu 528 kwa kila watu 100,000. Alisema kuwa hali hiyo, inadhihirisha
uhiotaji wa kupima na kugundua watu wengi zaidi.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa ni
rahisi kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu. Alizitaja dalili za kifua kikuu
kuwa ni kukohoa kwa wiki mbili au zaidi na homa za mara kwa mara hasa nyakati
za jioni. Dalili nyingine ni kutokwa na jasho lisilo la kawaida wakati wa usiku
hata kama kuna baridi. Kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu na kupungua
uzito ni miongoni mwa dalili hizo.
“Nawashukuru
sana wenzetu wa shirika la Save the Children kwa kuunga juhudi za Serikali za
kuwatambua na kuwapima wale watakaobainika kuwa na dalili za kifua kikuu katika
jamii yetu” alisema mheshimiwa Masenza.
Alishauri kuwa mtu anapoona
mojawapo ya dalili hizi kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na
tiba. “Serikali bado inaendelea kutoa
dawa za kifua kikuu bila ya malipo yoyote. Dawa zinapatikana katika vituo vyote
vya umma na vile vya binafsi” alisisitiza mheshimiwa Masenza.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni