Na.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wadau wa uhifadhi wa mto Ruaha Mkuu wametakiwa
kuungana kuunusuru mto huo usikauke ili uendelee kutiririsha maji kwa maendeleo
endelevu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa uhifadhi kilichohusisha
wizara za sekta zinazohusiana na maji, wakuu wa mikoa, Wakuu wa wilaya, Wakururgenzi
wa Halmashauri na wakuu wa taasisi mbalimbali za serikali pamoja na vyombo vya ulinzi
na usalama uliofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akifungua kikao cha wadau wa uhifadhi wa Mto Ruaha Mkuu kutoka mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe na Dodoma, katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa |
“Wote tunafahamu kuwa rasilimali za maji hususani
mto ruaha ni muhimu kwa Taifa letu katika kufikia maendeleo endelevu, lakini
usimamizi wa rasilimali za maji bado unakabiliwa na changamoto nyingi.
Tunapaswa kushirikiana wadau wote kwa lengo la kuwezesha kusimamia matumizi
kuwa endelevu. Tusipo unganisha nguvu kutasababisha kukosekana kwa mtiririko
endelevu wa mto ruaha na hatimaye maji kukosekana kwa shughuli mbalimbali”
alisema Masenza.
Alisema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha
migogoro kati ya watumia maji mbalimbali katika eneo la bonde la mto ruaha mkuu.
Alikitaka kikao hicho kuwa jukwaa muhimu kwa watekelezaji na wafanya maamuzi
kwa ngazi ya taifa, mikoa na wilaya kujadiliana na kuafikiana na mikakati
inayoweza kuleta tija ili kurejesha mtiririko wa mto Ruaha Mkuu.
Alisema kuwa
pamoja na jitihada za mikoa, wilaya na halmashauri kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali kuhifadhi rasilimali maji bado mto ruaha mkuu haujarejea kwenye hali
yake ya awali. Kutokana na hali hiyo, alikitaka kikao hicho kuwa ni mwanzo wa
ukurasa mpya wa ushirikiano unao lenga kuboresha na kuimarisha usimamizi
endelevu wa maliasili kwa manufaa ya kizazi hiki na kizazi kijacho. Aliongeza
kuwa kikao hicho kinalenga kufikia dira ya maendeleo ya taifa, kuimarisha usimamizi
na uendelezaji wa rasilimali za maji na kuhakikisha kuongezeka kwa huduma kwa
wananchi ya kupata maji safi na salama ifikapo Mwaka 2025.
Ikumbukwe
kuwa mto Ruaha Mkuu ulikauka tangu mwaka 1993 na toka hapo haujarejea
kikamilifu kwenye hali yake ya awali.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni