Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia TASAF
Manispaa ya Iringa wametakiwa kutathmini manufaa waliyopata kupitia fedha
wanazopewa na mpango huo.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza
alipofanya ziara maalum ya kuwatembelea wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya
masikini katika mtaa wa Ngelewala uliopo Kata ya Mwangata Manispaa ya Iringa
leo.
Masenza alisema “kila
mnufaika anayepokea pesa za TASAF lazima ajitathmini, fedha hizo zimemsaidia
nini? Kama hakuna basi ujue ipo kasoro”. Alisema kuwa serikali inatoa pesa
hizo ili ziwasaidie wanufaika kuondoka katika hali duni ya maisha kuelekea hali
bora. Alishauri kuwa pesa hizo zitumike kwa uangalifu ili zilete matokeo
yaliyokusudiwa.
Mkuu wa mkoa aliwataka watendaji wa mitaa kuwa karibu na wanufaika
wa mpango wa kunusuru kaya masikini ili kuwasaidia na kuwashauri vizuri. “Ni jukumu la kila mtendaji wa mtaa kujua
hitaji la kila mnufaika wa TASAF. Wapo wanufaika wanaotaka kufuga lakini
hawajui wanaanzia wapi, wapo wanufaika wanaohitaji kulima lakini hawajui
waanzie wapi, hivyo kuwa nao karibu kutawasaidia kufikia malengo yao”
alisema Masenza.
Akiwasilisha taarifa fupi ya mpango wa kunusuru kaya masikini
TASAF awamu ya tatu, mratibu wa TASAF Manispaa ya Iringa, Lucy Mtafi alisema
kuwa mpango huo umelenga kuziwezesha kaya masikini kupata mahitaji ya msingi na
fursa za kuongeza kipato, kulinda rasilimali zao na kuweka akiba kwa ajili ya
kujiletea maendeleo na hatimae kujitoa katika umasikini.
Mtafi alisema kuwa mitaa ya Mawelewele na Ngelewala inayotembelewa
na mkuu wa mkoa ina wanufaika 77 ambao walipokea ruzuku ya shilingi 28,928,000.
Akiongelea mafanikio yaliyopatikana, mratibu wa TASAF Manispaa ya Iringa,
aliyataja kuwa ni kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni kutoka 80%
hadi 99%.
Aliongeza kuwa wazazi wamemudu kununua mahitaji ya watoto ya shule. Mafanikio
mengine aliyataja kuwa ni mahudhurio ya kupima watoto kliniki yameongezeka kwa
90% na elimu ya lishe bora imetolewa kwa akina mama wanapohudhuria kliniki.
Jumla ya kaya 2,302 zimejiunga na mfuko wa tiba kwa kadi (TIKA) na wanufaika wa
wamemudu kupata mahitaji ya msingi kama milo mitatu kwa siku. Mengine ni
wanufaika kuanzisha biashara ndogondogo na ufugaji wa kuku na nguruwe.
Mpango wa kunusuru kaya masikini katika Manispaa ya Iringa
ulizinduliwa tarehe 6/1/2015.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni